Wakuu wa Polisi watakiwa kuzidisha mapambano dhidi ya uhalifu

0
260

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Polisi katika nchi za Mashariki mwa Afrika kuweka mikakati thabiti ya kukabiliana na magenge yote ya uhalifu unaovuka mipaka.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo jijini Arusha, wakati akifungua mkutano mkuu wa 21 wa Shirikisho la Wakuu wa Polisi Mashariki mwa Afrika.

Pia amewataka kudumishwa kwa ushirikiano miongoni mwa Watendaji, kwa kuwa ushirikiano ni moja ya mbinu kubwa zitakazosaidia kuzuia vitendo vya uhalifu.

Kuhusu vitendo vya rushwa, amewataka Wakuu hao wa Polisi katika nchi za Mashariki mwa Afrika kuongeza mapambano dhidi ya vitendo hivyo, kwa kuwa vinarudisha nyuma maendeleo katika nchi hizo.

Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini Simon Sirro ambaye amekabidhiwa Uenyekiti wa EAPCCO amesema kuwa, atashirikiana na viongozi wenzake ili kuhakikisha hali ya amani na utulivu inaendelea kuwepo kwenye nchi zao.

Shirikisho la Wakuu wa Polisi Mashariki mwa Afrika linaundwa na nchi 14 ambazo ni Tanzania, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), Djibouti, Kenya, Sudan, Sudan Kusini, Somalia, Rwanda, Uganda, Shelisheli, Comoro, Eritrea na Ethiopia.