Wakuu wa mikoa watakiwa kufanya uhakiki wa takwimu za operesheni anwani za Makazi

0
159

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape NNauye amewataka wakuu wa mikoa yote 31 nchini kufanya uhakiki wa takwimu za operesheni ya Anwani za Makazi katika mikoa yao hasa katika kipengele cha usimikaji wa miundombinu ya nguzo zenye majina ya barabara na mitaa pamoja na namba za nyumba.

Akizungumza katika kikao kazi na Wakuu wa Mikoa kilichofanyika leo Mei 24, jijini Dodoma Waziri Nape amesema kuwa uhakiki huo ni muhimu kwa kuwa takwimu za usimikaji wa miundombinu hiyo zinaonesha zipo chini ukilinganisha na uhalisia wa kilichotekelezeka katika mikoa ambayo kwa nyakati tofauti yeye binafsi pamoja na viongozi wengine walipita kukagua na kuridhika na utekelezaji

Ameongeza kuwa ifikapo siku ya Ijumaa Mei 27, Wizara hiyo itakuwa imepeleka fedha kwenye mikoa yote kwa ajili ya kufanya zoezi la uhakiki na kuweka takwimu sawa kulingana na uhalisia ili taarifa itakayowasilishwa ikiwa imesainiwa na Mkuu wa Mkoa husika iwe sahihi na ndio itakayokabidhiwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

“Ukiangalia hali ya takwimu kwa mfano mkoa wa Lindi inaonekana ni asilimia mbili tu ya physical signs ndio imetekelezwa, lakini uhalisia haupo hivyo kwa kuwa nimepita mikoa mingi hadi Zanzibar nimejionea lakini bado takwimu zinaleta utata hivyo niwaombeni sana twendeni tukahakiki ili sisi na nyie tuzungumze lugha moja kwa kupata takwimu halisi”, Amezungumza Waziri Nape.

Aidha Waziri Nape ametumia kikao hicho kupenyeza ajenda ya Wizara anayoisimamia ya kuipeleka nchi katika uchumi wa kidijitali ambapo Wizara hiyo imejipanga kufanya semina kwa wakuu wa mikoa na makatibu tawala ili kuzungumzia uchumi wa kidijitali unaendaje, nini kinatakiwa kufanyika na maeneo wanayopaswa kushiriki.

Kwa Upande wa Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) David Silinde amewataka Wakuu wa Mikoa kusimamia Kanuni za utekelezaji wa Anwani za Makazi ambazo ndio msingi wa utekelezaji wa zoezi hilo ikiwa ni pamoja na kuwabana watendaji kutumia fedha za mapato ya ndani bila kuathiri wala kutumia fedha zilizotengwa kwa ajili ya miradi mingine ya maendeleo.