Wakuu wa mikoa waipa kongole TBC

0
135

Baadhi ya wakuu wa mikoa ya Tanzania Bara waliotembelea ofisi za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) zilizopo Mikocheni mkoa wa Dar es Salaam, wamelipongeza shirika hilo kwa kuboresha matangazo yake pamoja na studio za kurushia matangazo hayo.

Akizungumza kwa niaba ya Wakuu hao wa mikoa, mkuu wa mkoa wa Arusha John Mongella amesema, pamoja na maboresho hayo ni vema TBC ikaendelea kusimamia weledi kama chombo cha umma ili vyombo vingine vya habari viige kutoka shirika hilo.

Pia ameitaka TBC iendelee kuonesha maendeleo ya miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa na Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TBC Dkt. Ayub Rioba Chacha amesema maboresho yanayoendelea katika kipindi cha Jambo Tanzania, TBC2 na kuanzishwa kwa chaneli ya kiingereza ya TBC yasaidia kutangaza habari nyingi zaidi kutoka mikoani, utalii na kuitangaza Tanzania Kimataifa.

Wakuu hao wa mikoa walioitembelea TBC ni Adam Malima ambaye ni mkuu wa mkoa wa Tanga, Dkt. Batilda Burian – mkuu wa mkoa wa Tabora, Joseph Mkirikiti wa Rukwa, Queen Sendiga – mkuu wa mkoa wa Iringa na Zainab Telack ambaye ni mkuu wa mkoa wa Lindi.

Wengine ni John Mongella – mkuu wa mkoa wa Arusha, Juma Homera ambaye ni mkuu wa mkoa wa Mbeya, mkuu wa mkoa wa Katavi – Mwanamvua Mrindoko na Abubakar Kunenge – mkuu wa mkoa wa Pwani.