Wakuu wa mikoa kujifunza Dodoma kupanga Machinga

0
423

Wakuu wa mikoa yenye halmashauri zenye hadhi ya majiji nchini wametakiwa kutumia mbinu inayotumika katika ujenzi wa soko la Wafanyabiashara wadogo (Machinga Complex) katika eneo la Bahi Road mkoani Dodoma.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Innocent Bashungwa wakati wa ziara yake pamoja na wakuu wa mikoa, Makatibu Tawala na Wakurugenzi wa mikoa yenye hadhi ya majiji kutembelea ujenzi wa soko hilo.

Akizungumza na Viongozi hao, Waziri Bashungwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametambua sekta ya machinga kuwa rasmi, hivyo kwa sasa wanaenda na maono yake ya kuhakikisha wanajengewa mazingira rafiki.

“Napongeza ubunifu uliofanyika kwenye soko hili la machinga na namna jiji lilivyotafsiri maono ya Rais kwa kubuni masuala haya hii ni fursa kwa Viongozi wengine wa mikoa yenye hadhi ya majiji kama Tanga, Arusha, Mwanza, Mbeya kujifunza kwa gharama ndogo hapa hapa nchini,” amesema Waziri Bashungwa

Amewataka Viongozi hao kupeleka elimu waliyojifunza kwenye soko hilo kwenye maeneo yao na kuhakikisha wanawashirikisha Machinga kwenye ujenzi wa miradi hiyo ambayo itatekelezwa kwenye mikoa yenye hadhi ya majiji nchini.