Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Ummy Mwalimu amewasimamisha kazi Wakurugenzi Watendaji wa halmashauri za wilaya ya Temeke mkoani Dar es salaam na Sumbawanga mkoani Rukwa, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili.
Mkurugenzi wa halmashauri ya manispaa ya Temeke Lusubilo Mwakabibi amesimamishwa kazi baada ya Waziri Ummy kupokea malalamiko na tuhuma za mwenendo usiofaa, matumizi mabaya ya madaraka, ubadhirifu na usimamizi usioridhisha wa miradi ya maendeleo katika halmashauri hiyo.
Waziri Ummy amemsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga, -Nyangi Msemakweli kutokana na tuhuma za ubadhirifu, usimamizi mbovu wa miradi ya maendeleo na mahusiano yasiyoridhisha na viongozi wenzake.
Kufuatia tuhuma zinazowakabili Wakurugenzi hao wa halmashauri za Temeke na Sumbawanga, Waziri Ummy amemuagiza Katibu MkuuTAMISEMI kupeleka timu za uchunguzi mara moja katika halmashauri hizo.