Wakulima Sikonge washauriwa kutolima pamba kwa sasa

0
220

Wakulima wa wilaya ya Sikonge  mkoani Tabora ambao wanataka kulima zao la Pamba wameshauriwa  kuwa wavumilivu,  hadi hapo utafiti utakapokamika ili Serikali ijiridhishe kama tishio la mdudu aina ya Funza Mwekundu halipo katika maeneo jirani yaliyopigwa marufuku kulima zao hilo.

Ushauri huo umetolewa wilayani Sikonge na Mkuu wa mkoa wa Tabora, –  Aggrey Mwanri,  wakati wa kikao cha robo ya kwanza cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya wilaya hiyo.

Mwanri  amewaambia Madiwani wa Halmashauri hiyo ya wilaya ya Sikonge kuwa,  wizara ya Kilimo iliweka karantini kwa wilaya zinazopakana na mikoa ya Rukwa na Mbeya kutolima pamba kutokana na kuwepo  Funza Wekundu wanaoshambulia zao hilo.

Amesisitiza kuwa, hawezi kuruhusu watu walime  zao hilo hadi hapo wataalamu wa Wizara ya Kilimo watakapokwenda wilayani humo kujiridhisha na kutoa tamko kuhusu kutokuwepo kwa tishio la mdudu huyo,  na amewaomba Madiwani kutowahamasisha Wananchi kulima zao hilo la pamba kabla hawajapata msimamo wa Serikali ili wasije kupata hasara.

Kwa mujibu wa Mwanri, kitendo cha kuruhusu kulimwa kwa zao hilo la Pamba  kabla ya matokeo ya wataalamu  kinaweza kusababisha hasara kubwa katika maeneo ya ndani na nje ya mkoa wa Tabora ambapo Funza huyo Mwekundu anaweza kusabambaa hata katika maeneo ambayo alikuwa hayupo.

Awali Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Sikonge, – Peter Nzalalila aliishauri Serikali iwaruhusu walime  pamba kama zao mbadala ya tumbaku, ambayo inapigwa vita Kimataifa.

Nzalalila alitoa ombi hilo kwa madai kuwa,  maeneo ya jirani na wilaya hiyo ambayo yalikuwa yamepigwa marufuku wameanza kulima  Pamba na wana Vyama Vya Msingi vya zao hilo.