Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, ameungana na wake wa Viongozi mbalimbali kusherehekea miaka Kumi ya Umoja wa Wake wa Viongozi uitwao New Millenium Women’s Group, kwa kutoa misaada katika kituo cha kulea Wazee cha Nunge kilichopo Kigamboni jijini Dar es salaam.
Mama magufuli, ambaye aliongozana na Mlezi wa Umoja huo Mke wa Waziri Mkuu Mary Majaliwa, Mwenyekiti wa Umoja huo Mke wa Waziri Mkuu Mstaafu Tunu Pinda na Mama Asina Kawawa, kwa pamoja wametoa misaada mbalimbali ikiwa ni pamoja na chakula na nguo.
Wakiwa katika kituo hicho cha kulea Wazee cha Nunge, Mama Magufuli amechangia gypsum 178 huku Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan akituma mchango wa Shilingi Milioni Tano kwa ajili ya ukarabati wa Bwalo katika kituo hicho kikongwe ambacho kwa sasa kinakaliwa na Wazee 26.
Umoja huo wa New Millenium Women’s Group umechangia ujenzi wa mnara wa kisima cha maji kwa gharama ya Shilingi Milioni 1.9, pamoja na vyakula na nguo vyenye thamani ya Shilingi Milioni Tatu.