Wajasiriamali Ruangwa wakabidhiwa mikopo

0
107

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekabidhi mikopo ya zaidi ya shilingi milioni 250 iliyotolewa na halmashauri ya wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 kwa vikundi 27 vyenye wanufaika 196.

Kati ya vikundi hivyo, vya wanawake ni 14 ambavyo vimepewa mkopo wa zaidi ya shilingi milioni 36, nane vya vijana vimepata mkopo wa zaidi ya shilingi milioni 200 na vikundi vitatu vya watu wenye ulemavu ambavyo vimekabidhiwa mkopo wa zaidi ya shilingi milioni 6.5.

Akizungumza na wakazi wa kata ya Mandawa wilayani Ruangwa baada ya kukabidhi mikopo hiyo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametumia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Ruangwa kwa matumizi mazuri ya asilimia 10 ya makusanyo yao ya ndani ambayo yanatakiwa yatolewe mkopo kwa vikundi vya vijana (asilimia nne), wanawake (asilimia nne) na wenye ulemavu (asilimia mbili).

Amesema uamuzi wa halmashauri hiyo kutoa mkopo huo utaviwezesha vikundi hivyo kuongeza mitaji na uwezo wa kuendeleza shughuli zao za ujasiriamali.

“Vikundi vimewezeshwa kwa kuongezewa mitaji itakayoviwezesha kuzalisha kwa tija na kuweza kurejesha mikopo kwa wakati ili waweze kukopeshwa wengine.” amesema Waziri Mkuu

Naye Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Frank Chonya amesema, kati ya fedha hizo zaidi ya shilingi milioni 210 zimetolewa kwa vikundi sita vya kimkakati ambapo kati yake vikundi vitatu vya vijana vinavyojishughulisha na usafirishaji wa abiria wa pikipiki vyenye wanufaika 20 vimepewa mkopo wa zaidi ya shilingi milioni 57 zilizotumika kununua pikipiki 20.