Waitara atoa uamuzi wa fedha za mfuko wa Jimbo la Hai

0
233

Naibu Waziri wa TAMISEMI, Mwita Waitara amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya kutumia fedha za mfuko wa Jimbo la Hai ambazo zimekaa bila kutumika kwa kipindi cha miaka miwili.

Akitoa maagizo hayo Januari 8 mwaka huu alipokuwa akizungumza na watumishi na wakazi wa wilaya hiyo Waitara amesema kuwa fedha hizo TZS 42 milioni zilitolewa katika mwaka wa fedha 2018/19 lakini hadi sasa hazijapangiwa matumizi jambo ambalo si sahihi.

Akiwa katika Kijiji cha Longoi alipokwenda kutembelea ujenzi wa kituo cha afya amesema kuwa mkuu wa wilaya pamoja na mkurugenzi ndio wenye mamlaka ya kupanga matumizi ya fedha za jimbo na sio mbunge kama ambavyo jimbo hilo linaloongozwa na Mwenyekiti wa CHADEMA (Taifa), Freeman Mbowe limekuwa likifanya.

Ameongeza kuwa Mbowe hatakiwi kupanga matumizi ya fedha hizo bali kazi yake ni kuchukua matatizo ya wananchi na kuyawasilisha bungeni.

Fedha za mfuko wa jimbo hutolewa ili kuchochea shughuli za maendeleo katika jimbo husika, na hivyo Waitara amemtaka mkuu wa wilaya na mkurugenzi kutawanya fedha hizo katika miradi ya maendeleo ndani ya jimbo. “Muagize Mkurugenzi atawanye fedha hizo kwenye miradi, wananchi wanaweza kuwasilisha maombi yao, na kazi yako (DC) uhakikishe zinatumika kama zinavyotakiwa,” amesema Waitara akitoa maagizo kwa DC Ole Sabaya

Akizungumza katika mkutano huo DC Sabaya alisema mtu yeyote atakayetumia vibaya fedha za wananchi atamfyatulia mbali, kwani tayari amepewa mamlaka na Naibu Waziri wa TAMISEMI.