Waitara aitaka ATCL kuboresha huduma zake

0
146

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mwita Waitara, amelitaka Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kuhakikisha linaboresha huduma zake, ili kuendelea kutoa huduma bora kwa Watanzania.

Akizungumza mkoani Dar es salaam mara baada ya mkutano wake na Menejimenti ya ATCL, Naibu Waziri Waitara amesema kwa sasa Watanzania wanaliamini shirika hilo, hivyo ni vema likaboresha huduma zake.

Amesema kuwa kwa sasa shirika hilo linaaminiwa na Watanzania wengi kutokana na ubora wa huduma zake, na hivyo kulitaka kuboresha zaidi huduma hizo na kupanua wigo wa safari zake.

Kuhusu kubadilika mara kwa mara kwa ratiba za safari za ndege za ATCL, Naibu Waziri Waitara amelitka shirika hilo kutoa taarifa za mabadiliko ya safari kwa wateja pindi yanapotokea, ili kuepusha usumbufu huku akiwaomba Watanzania kuwa wavumilivu wanapopatiwa taarifa za mabadiliko ya safari zao.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa ATCL Mhandisi Ladislaus Matindi amesema mara nyingi ratiba za safari za ndege za ATCL zimekuwa zikibadilika kutokana na ushauri wa kiufundi ambao umekuwa ukitolewa.

Ziara ya Naibu Waziri Waitara kwenye ofisi za Shirika la Ndege Tanzania ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wanalifuatilia kwa karibu shirika hilo na kuliwezesha kuwahudumia Wananchi.