Wahariri wa habari watakiwa kuzingatia takwimu kwa usahihi

0
233

Wahariri wa vyombo vya habari nchini wametakiwa kuendelea kuzingatia matumizi ya takwimu rasmi katika kuelimisha umma kuhusu miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali.

Akifungua warsha ya Wahariri wa Habari jijini Dodoma, Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt Albina Chuwa amesema kuwa, dhamira ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ni kuendelea kuhakikisha kuwa Wananchi wanapata taarifa sahihi katika nyanja mbalimbali ikiwemo katika matumizi ya takwimu zinazozalishwa hapa nchini.

“NBS iko tayari kusaidia asasi za kiraia ili kuzalisha takwimu sahihi kwa kutumia miongozo na kanuni za ukusanyaji na uchakataji wa takwimu hizo kwa maslahi ya Wananchi”, amesisitiza Dkt Chuwa.

Amesema kuwa, takwimu ni suala la Kisayansi, hivyo linahitaji utaalamu katika kukusanya, kuzichakata na kuzitoa kwa maslahi ya Wananchi na Taifa kwa ujumla.

Kwa mujibu Dkt Chuwa, Ofisi hiyo itaendelea kuvijengea uwezo vyombo vya Habari ili viweze kuelimisha umma kwa kutoa taarifa sahihi na kutumia takwimu rasmi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala, Fedha na Masoko wa NBS, Daniel Andrew amesema kuwa, Ofisi hiyo inatambua umuhimu wa vyombo vya habari katika kuelimisha umma kuhusu masuala ya takwimu na kuchochea maendeleo.

Warsha hiyo imewashirikisha Wahariri wa vyombo vya habari kutoka mikoa mbalimbali nchini.