Wagonjwa wenye matatizo ya moyo washauriwa kuhudhuria kliniki

0
177

Wagonjwa wenye matatizo ya moyo, kisukari, shinikizo la juu la damu, figo na saratani wameshauriwa kuhudhuria kliniki zao bila kukosa, kwani kwa kufanya hivyo wataweza kuepuka kupata madhara ya kiafya ikiwa ni pamoja na kufariki dunia.

Ushauri huo umetolewa jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Profesa Mohamed Janabi  wakati akizungumza kuhusu kupungua kwa idadi ya wagonjwa wanaotibiwa katika taasisi hiyo tangu virusi vya corona vilipoingia nchini.

Profesa Janabi amesema  hivi sasa idadi ya wagonjwa wanaotibiwa katika taasisi hiyo imepungua kutoka mia tatu hadi hamsini kwa siku, na wagonjwa wanaolazwa idadi yao imepungua  kutoka mia moja na hamsini hadi kufikia thelathini kwa siku.

Amesema wao kama madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo hawaelewi hivi sasa wagonjwa hao ambao hawahudhurii kliniki wanatibiwa wapi kwa sasa, hali inayoleta hofu zaidi kuhusu hali za afya za wagonjwa hao ambao wanahitaji uangalizi wa karibu wa madaktari.

“Wote tunafahamu kuwa kutokana na tafiti mbalimbali zilizofanyika ulimwenguni zinaonesha wagonjwa wenye matatizo ya moyo, kisukari, shinikizo la juu la damu, figo, saratani na watu wenye umri mkubwa wa zaidi ya miaka 60 ndiyo wanaoathirika zaidi na ugonjwa wa corona, ikiwa  wagonjwa hawa hawatahudhuria kliniki  kama walivyopangiwa na madaktari wao wakipata maambukizi ya virusi vya corona  ni rahisi kwao kufariki dunia,” amesema Profesa Janabi.

Amewasisitiza wagonjwa wenye matatizo ya moyo kwenda kutibiwa kwenye Taasisi hiyo ya Moyo Jakaya Kikwete kwani taasisi hiyo imechukua tahadhari  zote za kuhakikisha wagonjwa hawapati maambukizi ya virusi vya corona wawapo hospitalini.