Wagonjwa 36 wafanyiwa upasuaji wa moyo

0
2550

Jumla ya wagonjwa 36  wamefanyiwa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua na bila kufungua kifua katika kambi maalum ya matibabu inayofanyika katika Taasisi ya Moyo  Jakaya Kikwete (JKCI).

Upasuaji huo unafanywa na madaktari bingwa wa moyo wa taasisi hiyo kwa kushirikiana na wenzao wa Shirika la Albalsam  Care & Care la nchini Saudi Arabia ambapo wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa kufungua kifua ni kumi na bila kufungua kifua kwa kutumia mtambo wa Cathlab kwa njia ya kutoboa tundu dogo katika  paja ni 26.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa JKCI, -Bashir Nyangasa amesema kuwa wagonjwa waliofanyiwa upasuaji hali zao zinaendelea vizuri na wengine wameshatoka katika chumba cha uangalizi maalum na kurudi wodini kwa ajili ya kufanya mazoezi pamoja na matibabu.

“Tunafanya upasuaji wa kubadilisha valvu kwa wagonjwa ambao  valvu zao hazifanyi kazi vizuri, kubadilisha  mishipa ya moyo inayosafirisha damu kutoka mishipa mikubwa kwenda kwenye mzunguko wa moyo na kuziba matundu kwenye moyo kwa watu waliozaliwa na matundu hayo”, amesema Dkt Nyangasa.

“Katika kambi hii tumemfanyia upasuaji wa kupandikiza mshipa wa damu kutoka kwenye mguu na kuuweka kwenye moyo mgonjwa aliyekuwa na maradhi mawili ya moyo ambayo  ni kuziba kwa mishipa ya damu na mlango mkubwa wa moyo”, ameongeza Dkt Nyangasa.

Kwa upande wake  daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu kutoka Shirika la Albalsam Care and Care la nchini Saudi Arabia,- Emad Bukhari ameipongeza serikali ya Tanzania kwa kuwekeza  katika vifaa vya kisasa vya matibabu ya moyo.

“Kuwepo kwa mashine hizi za kisasa, wataalam pamoja na huduma nzuri  za kibingwa katika Taasisi hii, kumeifanya  kutambulika kimataifa na  hivyo kuzifanya taasisi zinazotibu magonjwa ya moyo Duniani kuja mahali hapa kutoa huduma kwa wananchi”, amesema Dkt Bukhari.

Kambi hiyo maalum ya matibabu inayofanyika katika Taasisi ya Moyo  ya Jakaya Kikwete, inafanyika kwa pamoja na utoaji wa elimu na ubadilishanaji wa ujuzi wa kazi ambao umewajengea uwezo madaktari, wauguzi pamoja na wataalamu wa mashine za moyo.