Wafikishwa mahakamani kwa tuhuma za mauaji

0
186

Na, Emmanuel Samwel TBC

Victoria Mseka na Mawazo Hassan wote wakazi wa Msakuzi wilayani Ubungo mkoani Dar es salaam, wamefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi wilaya ya Kinondoni wakikabiliwa na shtaka la mauaji.

Victoria na mwenzake wamefikishwa katika mahakama hiyo na kusomewa shtaka linalowakabili na wakili wa Serikali Benson Mwaitenda mbele ya hakimu mkazi wa mahakama hiyo Happy Kikoga.

Wakili wa Serikali Mwaitenda amedai kuwa, washtakiwa hao Januari 26 mwaka huu katika eneo la Msakuzi wilayani Ubungo mkoani Dar es salaam, walimuua Sauda Likiwa kinyume na makosa ya jinai kifungu cha 196 na 197 ya sheria ya makosa ya jinai ya mwaka 2019.

Amedai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika, hivyo kuomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya kutajwa kwa shauri hilo.

Awali kabla ya washtakiwa hao kusomewa shtaka lao, hawakuruhusiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 6 mwaka huu itakapotajwa na washtakiwa wote wamepelekwa rumande.