Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete watakiwa kujiendeleza kielimu

0
1136

Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete -JKCI wametakiwa kujiendeleza kielimu ili waweze kutoa huduma bora zaidi na za kisasa  kwa wagonjwa.

Rai hiyo imetolewa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Profesa Mohamed Janabi wakati akizungumza katika kikao cha wafanyakazi kilichofanyika Jijini Dar es Salaam.

Profesa Janabi amesema utoaji wa huduma bora kwa wagonjwa na wananchi unaendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia hivyo basi ni jukumu la wafanyakazi hao kuhakikisha wanajiendeleza kielimu   kwa njia ya mtandao, elimu ya masafa marefu au kwenda darasani.

Pia amewahimiza wafanyakazi hao kufanya kazi kwa bidii, kuwahi kazini na kutumia muda wao wa kazi  kutoa huduma kwa wananchi na si vinginevyo huku wakifuata sheria na taratibu za utumishi wa umma na maadili ya kazi zao.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uuguzi Robert Mallya amesema kurugenzi yake itaendelea kutoa mafunzo kwa maafisa uuguzi ya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wa moyo ili wagonjwa wanaotibiwa katika taasisi hiyo waendelee kupewa huduma bora zaidi ya kiwango cha kimataifa.