Wafanyakazi wa kada ya kati Zanzibar kuongezewa mishahara

0
254

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi amesema Serikali ina mpango wa kuongeza kima cha mshahara kwa Wafanyakazi wa kada ya kati, pindi hali ya uchumi itakapoimarika.

Dkt. Mwinyi ameyasema hayo wakati wa sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani, zilizofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul – Wakil Kikwajuni jijini Zanzibar.

Amesema Wafanyakazi wa kada hiyo ni muhimu katika maendeleo ya Taifa kwa vile ndio yenye Wafanyakazi wengi wakiwemo Walimu, Watumishi wa afya na wengineo ambao hivi sasa wanalipwa mishahara duni.

Kwa mujibu wa Rais Dkt. Mwinyi, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar awamu ya saba ilipanga kuongeza mishahara ya Wafanyakazi wa ngazi zote kwa awamu tatu, lakini jambo hilo limeshindikana kutokana na janga Corona ambalo limeathiri ukusanyaji wa mapato.

Amefafanua kuwa utaratibu huo wa kuongeza mishahara umeishia kwa Wafanyakazi wa kima cha chini, ambao mishahara yao imeongezwa na kufikia shilingi laki tatu kwa mwezi.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani kwa mwaka huu huko Zanzibar ni “Uwajibikaji na Haki ndio msingi wa maendeleo ya Zanzibar”.