Wafanyabiashara kizimbani kwa utakatishaji fedha

0
224

Wakurugenzi wawili wa Kampuni ya Vinywaji vikali (BEVCO) akiwemo raia wa Ufaransa, Melaine Philippe wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na makosa 45, ikiwemo kosa la utakatishaji fedha zaidi shilingi bilioni moja 1.6

Mbali ya Melaine mshitakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Ntemi Masanja.

Washitakiwa hao ambao wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 87 ya mwaka 2020, wamefikishwa mahakamani hapo na maafisa wa Takukuru na kusomewa mashitaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama ya Kisutu Godfrey Isaya.

Akiwasomea mashtaka yanayowakabili, wakili wa serikali, Maghela Ndimbo amedai washtakiwa hao wametenda makosa hayo kwa nyakati tofauti kati ya Oktoba 2017 na Juni 31, 2020 maeneo tofauti ya jiji la Dar es Salaam.

Kughushi, Kukwepa Kodi, Kuwasilisha Nyaraka za Uongo, Kuisababishia hasara Mamlaka ya mapato (TRA) na Utakatishaji fedha.

Katika kosa la utakatishaji fedha, washitakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo maeneo tofauti jijini Dar es Salaam katika tarehe tajwa wakati wakijua kufanya hivyo ni kosa la kisheria.

Aidha baada ya kusomea mashtaka hayo, Wakili Ndimbo amedai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika hivyo kuomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili kutajwa kesi hiyo.

Hata hivyo Hakimu Isaya amedai kuwa washitakiwa hawaruhusiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, hivyo washtakiwa wamerudishwa rumande na kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 3, mwaka huu itakapotajwa.