MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imewahukumu wafanyabiashara wawili, Magdalena Uhwello na Halima Nsubuga, kulipa faini ya Sh Mil. 101 au kwenda jela miaka 20 baada ya kukiri kufanya biashara ya upatu na utakatishaji fedha.
Aidha, mahakama imetaifisha Dola za Marekani 124,433 zilizopo kwenye akaunti ya Equity Tanzania na Dola za Marekani 263,567 zilizopo kwenye akaunti ya Equity Uganda.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Kisutu, Vicky Mwaikambo, amesema baada ya washitakiwa kukiri makosa hayo na mahakama kuwatia hatiani, watapaswa kulipa faini ya Sh milioni moja au kifungo jela mwaka mmoja kwa kosa la kufanya biashara ya upatu na katika mashitaka ya utakatishaji fedha, washitakiwa watatakiwa kulipa faini ya Sh Milioni 100 au kifungo jela miaka 20.
Hakimu Mwaikambo amesema washitakiwa wakishindwa kulipa faini hiyo, adhabu itakwenda kwa pamoja hivyo watatakiwa kutumikia adhabu ya miaka 20 jela.
Pia amesema fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya washitakiwa zinataifishwa na kuwa mali ya serikali.
Kabla ya kutolewa adhabu, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, ameiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa washitakiwa ili iwe fundisho kwa wengine wanaotaka kujiingiza katika biashara hiyo na kuomba mahakama itaifishe fedha hizo.
Wakili wa Utetezi, Augustine Shio, ameiomba mahakama iwaonee huruma washitakiwa hao kwa sababu ni kina mama ambao wana watoto wadogo wanaowategemea na kwamba hawana kipato chochote.
Katika mashitaka ya kwanza inadaiwa, Aprili Mosi, 2017 na Juni 30, 2017 maeneo ya jiji la Dar es Salaam washitakiwa hao walikula njama kutenda kosa la kusimamia na kuendesha biashara ya upatu ambapo walikusanya fedha kutoka kwa watu mbalimbali ambazo walikuwa wakichangia kwa kuwaahidi kuwapatia faida watakayopata.
Inadaiwa Aprili 25, 2017 washitakiwa hao walificha chanzo halisi cha fedha haramu walihamisha Dola za Marekani 263,567 kwenda kwenye akaunti ya Equity Uganda.