Wadaiwa wa TTCL kukatiwa mawasiliano

0
121

Taasisi za Umma zinazodaiwa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) zimetakiwa kulipa madeni hayo hadi ifikapo mwishoni mwa mwezi Januari mwaka 2021, na endapo zitashindwa kufanya hivyo zitakatiwa mawasiliano.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt Faustine Ndugulile mara baada ya kuzungumza na Wafanyakazi wa TTCL jijini Dar es salaam.

“TTCL inadai Taasisi za umma zaidi ya Bilioni 30 na tunajua Kuna Taasisi zinakusanya fedha nyingi kwenye kazi zao Ila hawakumbuki kulipa madeni ya TTCL, hivyo nimemuagiza Mkurugenzi kuwaandikia barua wadaiwa wote ili ifikapo tarehe 31 Januari 2021 kusiwe na kisngizio kwa watakaokatiwa mawasiliano” amesema Dkt Ndugulile.

Ameongeza kuwa Rais Dkt John Magufuli ameanzisha wizara hiyo ili kuleta tija kwenye usimamizi wa huduma za mawasiliano na kukuza kipato kwa Taifa, hivyo watahakikisha usimamizi wa karibu unafanyika ili kutimiza lengo alilojiwekea Rais kupitia wizara hiyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Waziri Kindamba amesema wapo tayari kwenda na kasi ya Serikali, ili kuhakikisha malengo yote yaliyokusudiwa yanatekelezeka.

“Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt John Magufuli kwa kuunda wizara hii maalum, tunamaini itatusaidia kutimiza malengo na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa Watanzania na kukuza pato la Taifa,” ameeleza Kindamba.