Wadaiwa wa NHC watakiwa kulipa madeni yao

0
158

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), uwaandikie barua wapangaji wote wanaodaiwa kodi na shirika hilo na wahakikishe zimelipwa ifikapo Mei 30 mwaka huu.
 
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo jijini Dar es salaam wakati akizungumza na viongozi na wajumbe wa Bodi ya NHC.

“Orodha ya wadaiwa niliyonayo hapa ni kubwa na wengine inaonesha wamehama na wameondoka bila kumalizia kodi zao, hawa wote ni lazima tuwafuatilie na walipe madeni yao,” amesema Waziri Mkuu.
 
Amesema madeni ambayo taasisi za Serikali zinadaiwa yanafikia Shilingi Bilioni 4.3 na endapo zitalipwa zote, zitaisaidia NHC kuendelea na mpango wake wa ujenzi wa nyumba nafuu kwenye maeneo mbalimbali.

“Taasisi zote za Serikali ambazo zimepanga kwenye nyumba za shirika ni lazima zilipe madeni, chombo chochote cha Serikali kinaishi na bajeti, kwa hiyo hata kama wamejenga ya kwao, walipaswa walipe kabla hawajahama”, amefafanua Waziri Mkuu Majaliwa.
 
“Waandikieni barua wadaiwa wote ili walipe, tunaelekea mwishoni mwa bajeti ya mwaka huu, na hawa wote wawe wamelipa ifikapo tarehe 30 Mei, 2020, nami nipate orodha ya taasisi za Serikali zinazodaiwa ili niwafuatilie, nitawaita Makatibu Wakuu wao mmojammoja na hao wadaiwa binafsi wachukulieni hatua stahiki”, amesema Waziri Mkuu.