Wadaiwa wa kodi ya pango la ardhi Kilombero watakiwa kulipa madeni yao

0
203

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angelina Mabula , ameiagiza halmashauri ya wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro kuzifuatilia Taasisi za Serikali zinazodaiwa kodi ya pango la ardhi kwenye halmashauri hiyo, ili ziweze kulipa deni hilo ambalo ni zaidi ya Shilingi Bilioni 1.9.

 Dkt Mabula ametoa agizo hilo alipokutana na uongozi wa wilaya ya Kilombero pamoja na Watendaji wa Idara ya ardhi katika halmashauri ya wilaya hiyo na ile ya Mji wa Ifakara, wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa Idara ya ardhi mkoani Morogoro.

 ‘’Taasisi zinashindwa kulipa madeni na hazijachukuliwa hatua, haiwezekani deni lifikie zaidi ya Bilioni Moja, fuatilieni suala hili na mchukue hatua za kisheria” amesisitiza Naibu Waziri Mabula.

 Agizo hilo la Dkt Mabula linafuatia taarifa ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kilombero Mhandisi Stephano Kaliwa iliyoeleza kuwa, miongoni mwa wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi katika halmashauri hiyo ni Taasisi za Serikali zinazodaiwa zaidi ya Shilingi Bilioni 1.9.

Miongoni  mwa Taasisi hizo ni Shirika la Umeme Nchini (TANESCO),  linalodaiwa zaidi ya Shilingi Bilioni 1.7 katika maeneo yake inayomiliki ya Kidatu, Kihansi na Mlimba.