Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, ameagiza Wakala wa Majengo (TBA), kuhakikisha inakusanya deni la Shilingi Bilioni 81.5 wanazodai kwa wapangaji wao sambamba na kuwaondoa wadaiwa sugu katika nyumba hizo ili upatikanaji wa fedha hizo uweze kusaidia utekelezaji wa miradi mingine nchini.
“TBA simamieni sheria kwa yeyote asiyelipa kodi hata kama ni kiongozi, waandikieni notisi ya kulipa madeni yao na wasipolipa waondoeni, wapo wengine nje wanasubiri wapewe nyumba ili waweze kulipa kodi kwa wakati na tutatumia makusanyo hayo kujenga nyumba nyingine”,- amesisitiza Bashungwa.
Bashungwa ameyasema mkoani Dodoma wakati alipofanya ziara yake kwa mara ya kwanza katika ofisi hizo na kuzungumza na menejimenti ya TBA ambapo amesisitiza uwekezaji wenye tija kwa watumishi na Taifa kwa ujumla.
Aidha, Bashungwa ameagiza TBA kuhakikisha wanakuja na mikakati itakayosaidia kujenga nyumba za bei nafuu hasa kwa vijana wanaoajiriwa katika utumishi wa umma hususan Dodoma ili kuweza kumudu gharama za maisha.