Wachina waliompa rushwa bosi wa TRA wahukumiwa

0
340
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ronglan Intl Industry and Trade Co. Ltd, Zheng Rongman (50) na mkewe Ou Ya (47)

Raia wawili wa China, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ronglan Intl Industry and Trade Co. Ltd, Zheng Rongman (50) na mkewe Ou Ya (47) wamehukumiwa kulipa faini yenye thamani ya shilingi milioni 1 kila mmoja baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kutoa rushwa ya dola za kimarekani 5,000, sawa shilingi milioni 11.5 kwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dkt. Edwin Mhede.

Hukumu hiyo imetolewa leo Februari 26, 2020 na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambapo mbali na adhabu hiyo mahakama imetaifisha fedha hizo, shilingi 11.5 milioni, kuwa mali ya serikali.

Wanandoa hao walifikishwa mahakamani Februari 25 na kusomewa shtaka moja la kutoa rushwa ambalo walikiri kulitenda Februari 24 katika ofisi za Makao Makuu ya TRA, jijini Dar es Salaam.

Wawili hao walitaka kumshawishi Dkt Mhede ili TRA awasaidie kampuni yao isilipe kodi ya shilingi bilioni 1.3.

Rongman na mkewe ni wakazi wa Mafinga mkoani Iringa.