Ofisi ya Bunge la Tanzania imekanusha taarifa ya upotoshaji inayosambaa mitandaoni kuwa wabunge ambao hawatachanja chanjo ya UVIKO-19 hawataruhusiwa kuingia bungeni.
Bunge limesema taarifa hiyo si ya kweli na kwamba Spika wa Bunge, Job Ndugai amekuwa akiwasisitiza wabunge kujitokeza kuchanja kwa hiari yao wenyewe.
Wakati vikao vya kamati za kudumu za bunge vikitarajiwa kuanza Jumatatu Agosti 16 mwaka huu, ofisi hiyo imesema imeandaa utaratibu wa kuwawezesha wabunge wote kupata chanjo katika viwanja vya bunge kwa hiari yao wenyewe.
Wabunge hao wameendelea kuhimizwa kutumia nafasi hiyo kupata chanjo kwa ajili ya kujikinga wao wenyewe na kuwakinga wengine dhidi ya maambukizi.
Mkutano wa nne wa Bunge utaanza Agosti 31, 2021.