Waandishi wa habari watatu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) wameshinda Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) mwaka 2019.
Waandishi hao walikabidhiwa tuzo hizo jana katika hafla iliyofanyika mkoani Tanga ikiwa ni kutambua mchango wao kwenye kuripoti habari mbalimbali.
Waandishi walioshinda ni Agness Mbapu (kwenye picha katikati) ambaye ameshinda tuzo ya kuripoti habari za afya ya uzazi, Tatu Abdallah (kushoto) ameshinda tuzo ya kuripoti habari za ubunifu wa maendeleo ya binadamu na Joselin Kitakwa (kulia) aliyeshinda tuzo ya kuripoti habari za kilimo na biashara ya kilimo.
Mbali na hao, mwandishi Betty Tesha amekuwa mshindi wa tatu katika kipengele cha kuripoti habari za afya ya uzazi.
Tuzo za EJAT hutolewa kwa waandishi wa magazeti, televisheni, redio na wa mitandaoni kwa kuwasilisha kazi zao bora zisizozidi tatu zinazopitiwa na EJAT kabla ya majina kutangazwa.