Waajiri watakiwa kuruhusu vyama vya Wafanyakazi

0
382

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira  na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama amewaagiza Waajiri kote nchini kuwaruhusu  Wafanyakazi wao  kuunda Vyama Vya  Wafanyakazi, ambavyo vitakua ni kiungo muhimu kati ya pande hizo Mbili.

Waziri Mhagama ametoa agizo hilo mkoani Mbeya,  wakati wa Sherehe za siku ya Wafanyakazi – Mei Mosi Kitaifa zinazofanyika kwenye Uwanja wa Sokoine.

Ameongeza kuwa mbali na Waajiri kuwaruhusu Wafanyakazi kuunda vyama vya Wafanyakazi, pia washirikiane na vyama hivyo kwa lengo la kuboresha mahusiano mazuri kazini, kuongeza ufanisi mahala pa kazi na kuondoa migogoro.

Waziri Mhagama amesema kuwa kwa upande wake,  serikali itaendelea kushirikiana na Wafanyakazi wote nchini  na kuhakikisha maslahi bora ya Wafanyakazi yanaendelea kuboreshwa.

Kauli mbiu ya siku ya Wafanyakazi Duniani Kitaifa kwa mwaka huu ni Tanzania ya Uchumi wa Kati inawezekana, Wakati wa Mishahara na Maslahi Bora ya Wafanyakazi ni sasa.

Mgeni rasmi katika sherehe hizo za Mei Mosi Kitaifa ni Rais John Magufuli na sherehe hizo zimehudhuria pia na viongozi wengine mbalimbali akiwemo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge Job Ndugai na Naibu Spika wa Bunge Dkt Tulia Ackson.