Vyama vya Ushirika wa kifedha 780 vyapewa Leseni

0
128

Mrajisi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini Dkt. Benson Ndiege amesema hadi kufikia mwezi Machi, 2023 jumla ya vyama vya ushirika wa kifedha 780 vyenye jumla ya Wanachama 1,731,237 vilikuwa vimepatiwa leseni kwa mujibu wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha Na. 10 ya mwaka 2018.

Dkt. Ndiege amesema vyama hivyo vina mtaji wa shilingi Trilioni 1.6 na akiba zenye thamani ya shilingi Bilioni 803 na amana zinazofikia shilingi Bilioni 713.6 huku mali za vyama hivyo zikifikia thamani ya shilingi Bilioni 945.3.

Mrajisi huyo wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini alikuwa akitoa tathmini ya tume hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita wakati wa maadhimisho ya Siku ya ushirika Duniani ambayo kwa mwaka wa tatu mtawalia yamefanyika kitaifa mkoani Tabora.