Vodafone kuipatia Tanzania bilioni 34

0
100

Kampuni ya Vodafone imeahidi kuipatia
Tanzania msaada wa shilingi bilioni 34, ili kuwezesha usafiri wa dharura kwa akina mama wajawazito.

Ahadi hiyo imetolewa katika kikao kilichofanyika kando ya mkutano wa Baraza Kuu la 77 la Umoja wa Mataifa (UNGA), jijini New York nchini Marekani.

Katika kikao hicho kilichokuwa chini ya Uenyekiti wa Mtendaji Mkuu wa Shirika la misaada la Marekani (USAID) Samantha Power, mkuu wa masuala ya kimataifa wa kampuni ya Vodafone Joachim Reiter aliwasilisha ahadi ya kutoa fedha hizo ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kukuza uchumi wa Tanzania.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango ambaye ameishukuru kampuni ya Vodafone kwa msaada huo.

Amesema takribani wanawake elfu nne na watoto elfu 65 hufariki dunia kila mwaka nchini Tanzania, huku kuchelewa kupata huduma za dharura ikiwa ni pamoja na usafiri wa dharura kukichangia sehemu ya vifo hivyo .

Naye Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ambaye naye ameshiriki katika kikao hicho amesema, msaada wa fedha hizo utaisaidia Tanzania kufikia malengo iliyojiwekea katika mkakati wa tano wa afya na Mpango Mkakati wa tatu wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto.