Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, – Constantine Kanyasu ameuagiza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuwaruhusu Wadau wa misitu nchini na ambao wana viwanda vya mbao, kuendelea kutumia mashine za zamani za kuchakata mbao huku wakijipanga kununua mashine za kisasa.
Naibu Waziri Kanyasu ametoa agizo hilo mkoani Kilimanjaro, alipokutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Wamiliki wa Viwanda vya mbao wa mikoa ya Kaskazini, – Ibrahimu Shoo.
Awali Shoo alimuomba Naibu Waziri Kanyasu wapatiwe muda wa kutosha kwa ajili ya kujipanga kununua mashine za kisasa za kuchakata mbao, baada ya kuzuiwa kutumia mashine za zamani kwa madai kuwa zimekuwa zikizalisha taka nyingi na hivyo kusababisha upotevu wa mbao.
Kufuatia ombi hilo la Shoo, Naibu Waziri huyo wa Maliasili na Utalii ameielekeza TFS iendelee kutoa leseni na mgao wa vitalu vya miti kwa wamiliki wa viwanda wenye mashine za zamani, ili kuwapatia fursa ya kujipanga kununua mashine zinazozalisha taka chache wakati wa uchakataji wa mbao.
Hata hivyo amewaeleza Wadau hao wa misitu nchini na ambao wana viwanda vya mbao kuwa uamuzi wa kubadili teknolojia ya kutumia mashine mpya zitakazosaidia kupunguza hasara ya upotevu mbao bado upo palepale.