Viwanda 148 vyaanzishwa Iringa

0
222

Jumla ya viwanda 148 vimeanzishwa mkoani Iringa kuanzia mwaka 2015 ambapo kati ya viwanda hivyo 138 ni vidogo, 7 vya kati na 3 ni vikubwa.

Takwimu hizo zimetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi wakati akitoa taarifa ya uwekezaji mkoani humo mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ambaye leo atazindua Mwongozo wa Uwekezaji mkoani humo.

Hapi amesema mafanikio hayo ni matokeo ya hatua mbalimbali za makusudi ambazo mkoa umechukua, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa kitengo maalum ambacho kimekuwa kikihudumia Wawekezaji mbalimbali.

Ameeleza kwa undani kuwa, kitengo hicho tangu kuanzishwa kwake kimehudumia Wawekezaji wakubwa 50, kwa kuwasaidia kupata ardhi kwa wakati, kutatua migogoro, kusaidia upatikanaji wa vibali na kuwasiliana na taasisi mbalimbali za serikali, lengo likiwa ni kuchochea uwekezaji.

Amemuahidi Waziri Mkuu kuwa mbali na kuvutia Wawekezaji, mkoa wa Iringa utaendelea kuwahudumia kwa karibu wawekezaji ambao tayari imewapata, ili wawe mabalozi wa kuvutia Wawekezaji wengine.