VIUATILIFU FEKI VYAMKERA MAKAMU WA RAIS

0
370
Makamu wa Rais Samia Suluh Hassan akisistiza jambo wakati akifungua maonesho ya 27 ya wakulima katika Viwanja vya Nyakabindi, Wilayani Bariadi Mkoani Simiyu

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ameiagiza Wizara ya Kilimo kushughulikia kasoro zilizopo katika upatikanaji wa pembejeo, hasa mbolea, mbegu na viuatilifu ili wakulima waweze kuzalisha kwa tija na kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo.

Makamu wa Rais Rais amesema kumekuwepo na malalamiko mengi kutoka kwa wakulima juu ya kupelekewa pembejeo ambazo hazina ubora na wakati mwingine kuwafikia zikiwa zimechelewa na kuwafanya wazalishe kidogo.

Mama Samia ameyasema hayo jana wakati akifungua rasmi maonyesho ya 27 ya Sikukuu ya Wakulima (Nane Nane) kitaifa Viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu.

Mhe.Samia ameitaka Wizara ya Kilimo kushirikiana na taasisi zilizoko chini ya wizara yake zinazohusika na jambo hilo, kuhakikisha wanawasimamia wazabuni wa pembejeo kutokana na kuwa tatizo sugu kwa wakulima nchi nzima.

“Suala la ucheleweshwaji na ubora wa pembejeo, ni suala ambalo limekuwa sugu sana, wizara lazima msimamie wazabuni mnaowapa fedha nyingi kusambaza mbolea, mbegu kwa wakulima, mara nyingi zinachelewa kuwafikia waulima na wakati mwingine zinakuwa chini ya kiwango.

“Malalamiko ya wakulima yamekuwa mengi, hawapati kwa wakati, lakini wakitumia wadudu hawafi, niagize wizara shughulikieni hili tatizo ili wakulima waweze kuzalisha vizuri na kwa tija,” alisema Samia.

Licha ya hali hiyo Makamu wa Rais amewataka watafiti nchini katika sekta ya kilimo kuhakikisha wanafikisha matokeo ya tafiti zao katika ngazi za chini kwa maofisa ugani na wadau wengine ili wakulima waweze kunufaika.

Amesema watafiti wengi wamekuwa wakifanya kazi nzuri na kupata mbegu bora zinazokinzana na magonjwa pamoja na mbegu zinazohimili mabadiliko ya tabia nchi na alisema tafiti hizo zimekuwa haziwafikii wakulima kama inavyotakiwa ili waweze kubadilika.

“Kumekuwepo na malalamiko juu ya operesheni hii, hasa kwenye ziwa letu hili la Victoria, sheria hazifuatwi, lakini pia hata Serikali inapoteza mapato yake, niagize wizara husika kulifanyia kazi jambo hili ili sheria ziweze kufuatwa kadiri inavyotakiwa,” amesema.

Mama Samia amewataka wataalamu wa mifugo kutumia maonyesho ya Nanenane mwaka huu kuhakikisha wanatoa elimu kwa wafugaji jinsi ya kufanya ufugaji endelevu wa kuvuna mifugo yao na kujiongezea kipato, ikiwa pamoja na kuondokana na migogoro ya wakulima na wafugaji.