Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa nchini kusimamia kikamilifu nidhamu na maadili katika maeneo yao ili dhamira ya serikali kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi itimie kwa wakati.
Akifunga mafunzo kwa viongozi hao jijini Dodoma, Waziri Jafo amesema kuwa jukumu la Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa nchini ni kuhakikisha kuwa agenda ya serikali na ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inatekelezwa kikamilifu kutokana na usimamizi wa nidhamu na uadilifu kote nchini.
“ Wakuu wa Mikoa kawekeni mkazo katika kusimamia masuala yanayolenga kuleta mageuzi katika maisha ya wananchi kwa kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora zinazoendana na dhamira ya Serikali ya kuwaletea wananchi maendeleo”, amesisitiza Waziri Jafo.
Amesema kuwa dhamira ya serikali ni kuendelea kuimarisha usimamizi wa miradi ya maendeleo ikiwemo ya ujenzi wa barabara katika majiji ya Arusha, Dar es salaam, Mwanza, Mbeya, Tanga na Dodoma ili kuimarisha na kuongeza tija katika majiji husika kutokana na kuimarishwa kwa miundombinu ya barabara.
Waziri Jafo pia amewataka viongozi hao kuhakikisha kuwa kero za wananchi zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati badala ya kusubiri viongozi wa kitaifa wafanye ziara katika maeneo husika na kutoa ufumbuzi .
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi Profesa Joseph Semboja amesema kuwa mafunzo hayo yatasaidia kujenga timu za utendaji na kuimarisha uwezo wa Wakuu hao wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa nchini katika ngazi ya mikoa.
Amesema kuwa viongozi hao wamejengewa uwezo ili waweze kuleta mageuzi makubwa katika utendaji wao na maeneo yao.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na kuratibiwa na Taasisi ya Uongozi pamoja na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa wakuu hao wa mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa nchini yamefanyika kwa muda wa siku tano Jijini Dodoma.
Mada mbalimbali zimewasilishwa wakati wa mafunzo hayo ikiwemo ile inayohusu dawa za Kulevya na namna serikali inavyofanya kazi.