Viongozi wa Dini wameombwa kuombea Taifa

0
154

Viongozi wa dini mkoani Kilimanjaro, wameombwa kuendelea kuliombea Taifa hasa katika kipindi hiki ambacho nchi na dunia kwa ujumla inakabiliwa na awamu ya tatu ya mambukizi ya ugonjwa wa korona.

Ombi hilo limetolewa na Mkuu wa mkoa huo Stephen Kagaigai, aliposhiriki misa ya Jumapili katika kanisa la Kilimanjaro Revival Templex -TAG.

Kagaigai amesema iko haja kwa viongozi hao kuendelea kuwasisitizia waumini wao kufuata miongozo inayotolewa na wizara ya afya juu ya kujikinga na ugonjwa huo.

” Viongozi wa dini nawaomba muhakikishe katika nyumba zenu za ibada waumini wanavaa barakoa, wananawa mikono kwa maji tiririka na sabuni pamoja na kutumia saniters”, amesema Kagaigai.

Amesema viongozi wa dini wanayo nafasi kubwa ya kuwaelimisha waumini wao kwani asilimia kubwa ya nyumba za ibada zimekuwa na misongamano hivyo tahadhari inahitajika.

Kwa upande wake, Mchungaji wa kanisa hilo Ron Swai, amesema kanisa litaendelea kushirikiana na serikali ya mkoa katika kukabiliana na korona pamoja na kuleta maendeleo ya mkoa huo.

Sauda Shimbo, Moshi