Viongozi wa CCM watakiwa kuzingatia katiba

0
944

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wahakikishe wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia katiba ya chama ili kuepusha migogoro kwenye maeneo yao.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo mkoani Kagera wakati akizungumza na viongozi wa CCM, wabunge pamoja na baadhi ya viongozi wa mkoa wa Kagera kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM ya mkoa huo.

Amesema kuwa chama chochote ambacho viongozi wake hawazingatii katiba lazima kiwe na migogoro, kwani uzingatiaji wa katiba ni miongoni mwa mambo yanayokitofautisha Chama Cha Mapinduzi na vyama vingine vya siasa nchini.

Waziri Mkuu ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Mlezi wa CCM mkoa wa Kagera amesema kuwa,  ni muhimu kwa viongozi hao kusoma na kuizingatia katiba ya chama kwa sababu inaelekeza misingi yote ya utendaji.

Amewasisitiza wanachama na wapenzi wa CCM kusoma katiba ya chama na kuzielewa kanuni, taratibu na sera ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Halkadhalika Waziri Mkuu Majaliwa ameonya kuwa serikali  haitazivumilia  baadhi ya  halmashauri ambazo zimeshindwa kuwasimamia watendaji wake  kukusanya mapato kwa mfumo wa kielektroniki.