Akihutubia mkutano wa Mifumo ya Chakula Afrika 2023 (AGRF) mkoani Dar es Salaam, Rais Samia Suluhu Hassan amependekeza Viongozi wa Afrika kufanya tathmini ya vipaumbele vilivyopo katika nchi zao ili kuleta suluhisho la changamoto zinazohusu mifumo na usalama wa chakula.
Rais Samia amesema ili kufikia lengo la kujadili kadhia za mifumo ya chakula na kubadilishana uzoefu wa namna ya kuendeleza minyororo ya thamani za bidhaa za kilimo na kujadili mipango ya kuimarisha usalama wa chakula barani Afrika, viongozi wa Afrika hawana budi kufanya tathmini ya vipaumbele vyao na kuvinasibisha na mahitaji ya sasa katika muktadha mpana wa kidunia.
Ameongeza kuwa kwa kufanya hivyo kutawezesha kuyafikia mageuzi yanayohitajika katika mifumo ya chakula na kuifanya sekta ya kilimo kuifikia Afrika inayotazamiwa.
Mkutano wa Mifumo ya Chakula Afrika 2023 (AGRF) ulioanza Septemba 05, 2023 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) utahitimishwa Septemba 08, 2023.