Vijana kupatiwa mashamba yenye hati

0
160

Rais Samia Suluhu Hassan amesema serikali imejipanga vema kuongeza ushiriki wa vijana katika sekta ya kilimo, kwa kuwapatia mashamba yenye hati zenye majina yao ama vikundi.

Rais Samia ameyasema hayo wakati wa sherehe za wakulima maarufu Nanenane kitaifa, zilizofanyika katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

Ameongeza kuwa, serikali imejipanga kuwaunga vijana katika huduma za mikopo yenye riba nafuu inayopatikana kwenye benki mbalimbali nchini, na kwamba fedha zipo tayari kwa ajili ya kutoa mikopo hiyo.

Kwa mujibu wa Rais Samia, serikali pia imejipanga kuhakikisha masoko yapo ya bidhaa mbalimbali zikazozalishwa na vijana.

Amesema ziara alizokuwa akizifanya nje ya nchi ni kwa ajili ya kutafuta soko la bidhaa zinazozalishwa nchini.

Rais Samia Suluhu Hassan amesema njia nyingine ya kuongeza fursa za ajira nchini ni kuwapa vijana vitalu ndani ya Ranchi za Taifa, ili waweze kujisuughulisha na ufugaji wenye tija.

Wakati wa sherehe hizo za Nanenane, Rais Samia amezindua mpango wa ruzuku ya mbolea kwa ajili ya wakulima nchini, ambao unatarajiwa kuanza kutumika rasmi tarehe 15 mwezi huu na pia ameshuhudia utiaji saini wa mikataba 21 ya skimu za umwagiliaji yenye thamani ya shilingi bilioni 182, inayotegemewa kutengeneza ajira kwa vijana takriban laki moja.