Vijana 97,000 wanufaika na mafunzo ya uanagenzi

0
270

Vijana 97, 000 wamenufaika na mafunzo ya uanagenzi yanayotolewa kupitia programu ya kukuza ujuzi iliyopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu inayolenga kufungua fursa nyingi za ajira kwa vijana nchini.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa ajira na ukuzaji ujuzi kutoka ofisi ya Waziri mkuu, Ally Msaki wakati akizungumzia program hiyo mkoani Dodoma na kueleza namna gani serikali inavyoendelea kuzalisha fursa za ajira kwa vijana kote nchini.

Aidha Msaki, amesema mafunzo hayo yalianza kutolewa mwaka 2017 kwenye vyuo vya ufundi 92 nchini na yanagharamiwa kwa asilimia 100 na serikali ya Tanzania.

Akibainisha kuhusu mafunzo hayo Msaki amesema, mafunzo ni ya miezi sita na fani zinazotolewa ni ufundi umeme wa majumbani na viwandani, umeme wa jua, useremala, ufundi magari, umeme wa magari, uchomeleaji na uungaji vyuma, utengenezaji wa vifaa vya aluminium, upishi, uhudumu wa hoteli na vinywaji, ushonaji, uchenjuaji wa madini, ufundi bomba, ufundi uashi, uwekaji wa terazo na marumaru, ufundi viyoyozi na majokofu.