Vigogo wa wilaya wasimamishwa kwa kuchelewesha miradi

0
156

Waziri wa TAMISEMI, Innocent Bashungwa amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa Kagera, Prof. Faustine Kamuzora kuwasimamisha kazi Afisa Manunuzi wa Wilaya Karagwe, Magreth Bukuku na Mkaguzi wa Ndani wa Wilaya Karagwe, Dickson Sabe kuanzia leo Juni 11, 2022 ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili.

Bashungwa amechukua hatua hiyo wakati akikagua ujenzi wa Hospitali  ya Wilaya Karagwe na kubaini ucheleweshwaji wa ujenzi wa majengo ya wodi ya wanaume, wodi ya wananamke, jengo la upasuaji na jengo la kuhifadhi maiti, chanzo chake kikiwa ni afisa manunuzi na mkaguzi wa ndani.

Amesema Serikali ilitoa shilingi milioni 800 na zipo kwenye akaunti ya halmahauri kwa ajili ya ujenzi wa majengo manne, lakini afisa manunuzi amekuwa na michakato isiyokuwa rasmi na kuomba kupewa fedha ili atoe tenda kwa wazabuni na kuchelewa kufanya maamuzi ya ununuzi wa vifaa.

Aidha, Bashungwa amesema mkaguzi wa ndani amekuwa akishiriki kusambaza vifaa katika miradi ikiwa ni pamoja ujenzi wa majengo ya hospitali ya wilaya badala ya kusimamia thamani fedha zinazoletwa katika halmashauri hiyo.

Naye,  Mkuu wa Mkoa Kagera, Meja Jenerali  Charles Mbuge amesemea katika eneo la mradi  hakuna vifaa vya ujenzi kama matofali, mchanga na vifaa vingine, jambo linalochangia kuchelewa kwa ujenzi.