Vigogo sita bodi ya wakulima wa chai Mponde mahakamani

0
2666

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini -TAKUKURU imewafikisha mahakamani vigogo sita wa bodi ya wakurugenzi wa kiwanda cha wakulima wa chai cha MPONDE kwa tuhuma za uhujumu uchumi.

Watuhumiwa hao wamefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi Mkoa wa TANGA na kusomewa mashtaka mawili yanayohusu uhujumu uchumi.

Waliofikishwa mahakamani hapo ni Nawab Mulla, Shahdad Mulla, William Shellukindo,Richard Mbughuni, Richard Madandi na Rajab Msagati.

Akisoma hati ya mashitaka, mwanasheria wa serikali, Seth Mkemwa akisaidiana na Magubo Waziri wameieleza mahakama kuwa kati ya mwaka 2000 na 2013 watuhumiwa wote kwa pamoja walikula njama na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya shilingi Bilioni 30.

Mkemwa alieleza kosa la kwanza la watuhumiwa hao kuwa kati ya January 2000 hadi desemba 2013 washtakiwa walikula njama na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya shilingi Bilioni 30.

Kosa la pili ni kuwa watuhumiwa hao mnamo Januari mwaka 2000 na Desemba 2013 kwa nia ovu wameidanganya Mamlaka ya Mapato Nchini -TRA kutaka msamaha wa kodi katika vifaa mbalimbali walivyodai kuviingiza kwa ajili ya wakulima wadogo wa chai jambo ambalo si kweli.