Vifungashio vilivyopigwa marufuku vyaendelea kutumika

0
465

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limesisitiza kuondoa sokoni vifungashio visivyo vya karatasi, na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi baada ya kubaini kuwa vifungashio vilivyopigwa marufuku vinaendelea kutumika.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt Samuel Gwamaka baada ya kutembelea kiwanda cha kutengeneza karatasi cha Mgololo (MPM) kilichopo wilayani Mufindi mkoani Iringa ili kujiridhisha na uzalishaji wa bidhaa hiyo ambayo ununuzi wake umekua si wa kuridhisha.

Dkt Gwamaka ameeleza kusikitishwa na kushuka kwa hali ya uzalishaji kiwandani hapo kutokana na kukosekana kwa soko la ndani.

Katika taarifa yake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda hicho, Mhandisi Gregory Chogo amesema kuwa, kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya mifuko mbadala isiyokidhi vigezo, uzalishaji wa kiwanda chake umeshuka kwa asilimia 15 kulinganisha na miaka miwili iliyopita.

Kutokana na ongezeko la matumizi ya mifuko iliyopigwa marufuku, NEMC imetahadharisha uingizaji wa mifuko mbadala kutoka nje ya nchi unaweza kuleta magonjwa ya mlipuko nchini, ikiwa ni pamoja na virusi vya corona ambavyo vimeendelea kuenea katika maeneo mbalimbali duniani.