Rais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa mkuu wa mkoa wa Morogoro, Adam Malima kufuatia vifo vya watu wawili katika ajali ya ndege.
Ajali hiyo imetokea leo Mei 18,2023 katika kiwanja cha ndege cha Matambwe kwenye Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na kusababisha vifo vya watu wawili na majeruhi wawili.
Kwa mujibu wa wizara ya Maliasili na Utalii, ndege hiyo aina ya Cessina 192 5H-FZS ikiwa na abiria watatu na rubani ilipata ajali wakati ikiruka katika kiwanja hicho.
Katika ajali hiyo askari wawili wamejeruhiwa na hali zao ni mbaya ambapo baada ya kuokolewa walikimbizwa zahanati kwa ajili ya kupatiwa huduma ya kwanza huku wakisubiri ndege ya kuwapeleka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi.
Aidha, miili ya marehemu imehifadhiwa kwa muda katika zahanati ya hifadhi hiyo.
Katika salamu zake Rais Samia amewapa pole wafiwa wote na kusema anaungana na familia hizo katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.