Vielelezo vinne vyakabidhiwa Mahakamani kesi ya Mbowe

0
199

Afisa wa Polisi katika Kitengo cha Uchunguzi wa Silaha na Milipuko katika ofisi ndogo ya makao makuu ya Polisi iliyoko Dar es Salaam, Coplo Khafidhi Adalah amekabidhi vielezo vinne vya ushahidi wake katika mahakama Kuu Divisheni ya makosa ya rushwa na Uhujumu Uchumi.

Coplo Adalah ambaye ni shahidi wa tatu kwa Upande wa Mashitaka katika kesi ya Uhujumu Uchumi na ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe na wenzake watatu amekabidhi vielelezo hivyo ambavyo katika ushahidi wa Awali vinadaiwa kukutwa kwa mshitakiwa wa pili Adam Kasekwa katika kesi hiyo ili vitumike kama vielelezo vya ushahidi wake mahakamani hapo.

Vielelezo hivyo vilivyowasilishwa na shahidi huyo mbele ya Jaji Joachim Tiganga ambaye anasikiliza shauri hilo ni pamoja na bastola moja,ripoti ya uchunguzi wa silaha, risasi moja na Maganda mawili ya risasi.

Akiongozwa na wakili wa Serikali Robert Kidando kutoa ushahidi wake, Shahidi huyo ameieleza Mahakama hiyo kuwa Novemba 25 mwaka 2020 alipokea bastola A 5340 ikiwa na risasi tatu kutoka ofisi ya DCI kwa ajili ya kuifanyia uchunguzi ambapo alitumia risasi mbili kati ya tatu ili kujua iwapo bastola hiyo inafanya kazi au laa!

Shahidi huyo amedai alikamilisha uchunguzi wa silaha hiyo Novemba 26 mwaka 2020 nakukabidhi ripoti yake kwa afande Swila ambaye anafanya kazi ofisi ya DCI Novemba 27, mwaka 2020 hivyo kuomba mahakama hiyo kupokea vielelezo hivyo kama sehemu ya ushahidi kwenye kesi hiyo.

Hata hivyo baada ya shahidi huyo kuhojiwa Upande wa Jamhuri na utetezi mahakama hiyo imeridhia kupokea vielelezo hivyo vyote vilivyowasilishwa na shahidi vitumike kama sehemu ya ushahidi kwenye kesi hiyo namba 16, ya Mwaka 2021.

Jaji Joachim Tiganga amepokea vielelezo hivyo kama kielelezo cha pili cha upande wa mashtaka baada ya shahidi huyo kuvisoma Mahakamani.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba Mosi mwaka huu ambapo mahakama itaendelea kupokea ushahidi kwa Shahidi kati ya 24 kwa Upande wa Jamhuri.