Rais John Magufuli amewaonya viongozi wa kisiasa kuacha vitendo vya kuwaweka ndani madaktari hata kwa makosa madogo, vitendo ambavyo amesema yeye hakubaliani navyo.
Rais ametoa kauli hiyo alipokuwa akihutubia mamia ya madaktari waliokusanyika katika ukumbi kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) ikiwa ni maadhmisho ya Siku ya Madaktari Tanzania mwaka 2020.
“Haifurahishi na wala haiji, mtu kila mahali akienda ni kuweka ndani. Nitoe wito kwa viongozi wengine wa kisiasa, tusiweke weke watu ndani,” amesema Rais Magufuli.
Hata hivyo Rais amesema kuwa onyo hilo alilolitoa sio kigezo cha kwamba madaktari hawatowekwa ndani endapo watatenda makosa, huku akitolea mfano wa daktari anayedaiwa kumbaka mjamzito na kusema kwamba, daktari anayefanya vitendo kama hivyo, hata akiwekwa ndani, madaktari wenzake wasilalamike.
Kuhusu wataalamu kutoka sekta nyingine amesema, “Na hii sio kwa madaktari tu, hata kwa wahandisi na walimu, haiwezekani kila mtu wewe unaweka ndani?”
Aidha, Rais amekiagiza Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kuwaonya na kuwachukulia hatua madaktari wachache wanaoshindwa kutumia taaluma zao vizuri, kabla hawajashughulikiwa na wanasiasa.
Katika siku hii ya madaktari, Rais Magufuli ameeleza kufurahishwa na mwenendo wa sekta ya afya nchini, ambapo mbali na kueleza mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya miaka minne iliyopita, ameahidi kutatua changamato zinazowakabili ikiwemo kutoa ajira, na kuwapatia jengo kwa ajili ya chama chao.