Kiwango cha uzalishaji wa mazao ya mifugo na uvuvi na matumizi yake kimeongezeka ukilinganisha na kile kilichokuwepo mwaka 2020.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah wakati akisoma taarifa ya wizara hiyo kwenye sherehe ya ufunguzi wa maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani ambayo kitaifa imefanyika mkoani Kilimanjaro kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Nelson Mandela iliyopo Pasua, Moshi.
“Kiwango cha uzalishaji wa samaki kupitia maji ya asili kwa mwaka 2021 kimefikia takribani tani 372,000 huku uzalishaji wa mazao hayo kwa ufugaji wa samaki ukifikia takribani tani 20,355 na wastani wa kiwango cha ulaji wa samaki kimeongezeka kutoka kilo 8.2 hadi kilo 8.5 kwa mtu kwa mwaka.” amesema Dkt. Tamatamah.
Kwa upande wa sekta ya Mifugo, Dkt. Tamatamah amesema kuwa kiwango cha uzalishaji wa nyama kimeongezeka hadi tani 738,166 kutoka tani 701,679 zilizozalishwa mwaka uliopita na kiwango cha uzalishaji wa maziwa kimefikia lita bilioni 3.4 kutoka lita bilioni 3.1 mwaka uliopita.
Dkt. Tamatamah amebainisha kuwa kuongezeka kwa kiwango hicho cha uzalishaji wa mazao ya mifugo na uvuvi kumetokana na dhamira ya serikali katika kuhakikisha wananchi wanaondokana na uhaba wa chakula na lishe bora hapa nchini.