UVIKO19: Rais aitaka JWTZ kujiweka tayari kwa chanjo

0
249

Rais Samia Suluhu Hassan amelipongeza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa namna ambavyo limekuwa likilinda mipaka ya Tanzania na kuiwakilisha nchi vizuri kimataifa katika ulinzi wa amani.

Rais ametoa pongezi hizo leo katika hafla ya makabidhiano ya miradi mbalimbali iliyotekelezwa na Ujerumani nchini ikiwemo Hospitali ya Kijeshi ya Magonjwa ya Mlipuko iliyopo kambi ya jeshi Lugalo mkoani Dar es Salaam.

Amesema serikali itaendelea kuliimarisha jeshi hilo ikiwa ni pamoja na kuangalia maslahi yao, na kueleza kwamba tayari amewapandisha vyeo baadhi ya maofisa wa jeshi hilo.

Aidha, amelitahadharisha jeshi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya UVIKO-19 na kuwataka wanajeshi kuwa tayari pindi watakapotakiwa kuchanjwa, kwani yeye kama kiongozi ameshaonesha mfano.

Amewatoa hofu kuwa chanjo hiyo haina madhara kama inavyodaiwa, kwani ingekuwa ndivyo, yeye kama kiongozi wa nchi asingeikimbilia.

Rais ametumia jukwaa hilo kuishukuru Ujerumani kwa ushirikiano wake na Tanzania ambao umewezesha kukamilika kwa miradi zaidi ya 10 ambayo imekabidhiwa kwa JWTZ.

Mbali na miradi hiyo, Ujerumani imeahidi kujenga hospitali kubwa ya kisasa mkoani Dodoma na kituo cha ulinzi wa amani eneo la Msata mkoani Pwani.