Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) mkoa wa Mtwara wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa ilani ya chama hicho kwa vitendo.
Wakizungumza wakati wanakabidhi maandamano ya amani ya kumkaribisha Rais Samia kwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas wamesema ilani ya CCM kwa mkoa wa Mtwara imejenga miradi mbalimbali ya maendeleo.
Aidha, wameitaja baadhi ya miradi ya maendeleo iliyojengwa mkoani Mtwara na inayoendelea kujengwa ni kukamilika kwa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini, upanuzi wa Bandari ya Mtwara upanuzi wa kiwanja wa ndege.
Miradi mingine ni kuanza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Mnivata- Tandahimba-Newala-Masasi ambapo wakandarasi wako site na uboreshaji wa miradi ya maji.
Akipokea maandamano hayo, Kanali Abbas amewataka wakazi wa Mtwara kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali za kuleta maendeleo pamoja na kuwataka kujitokeza kwa wingi kesho kwenye mapokezi ya Rais Samia anayetarajia kuanza ziara ya kikazi ya siku nne.