Utalii wa ndege waongezeka msitu wa Amani

0
2056

Idadi ya watalii wanaokwenda kutazama ndege katika hifadhi ya Msitu wa Amani wenye aina za ndege zaidi ya 400 uliopo Muheza Tanga, imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka, huku aina ya ndege inayovutia watalii wengi ikiwa ni ‘Kolokolo Domorefu’.

Akizungumza na TBC Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi hiyo Mwanaidi Kijazi amesema katikati ya mwaka jana na mwaka huu watalii 782 wamefika hifadhini hapo ambapo zaidi ya 200 kati yao walifika kwa ajili ya kutazama ndege hao adimu duniani na inaosemekana kuwa wapo katika hatari ya kutoweka.

Kutokana na hofu ya kutoweka kwa ndege hao serikali na wadau wa maendeleo ikiwemo taasisi ya Nature Tanzania wamezindua mradi maalum wa kumhifadhi ndege huyo.

Baadhi ya washiriki wa uzinduzi wa mradi huo wamesema kuwa watalii wengi hufika ili kukata kiu ya kumuona ndege huyo kabla hajatoweka duniani.

Imeelezwa kuwa aina nyingine ya ndege inayovutia watalii wengi ni Flamingo, huku ikielezwa kuwa Flamingo wote waliopo katika bara la Afrika asili yao ni Tanzania.