Upotevu wa milioni 231 wabainika Mvomero

0
236

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)  Innocent Bashungwa amebaini upotevu wa fedha na matumizi yasiyosahihi  ya shilingi milioni 231.84 katika ujenzi wa shule ya  Sekondari ya kumbukumbu ya Sokoine katika halmashauri ya wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.
 
Waziri Bashungwa amebaini upotevu huo wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika halmashauri ya wilaya Mvomero na kumtaka mkurugenzi wa halmashauri hiyo Hassan Njama  kutoa ufafanuzi.
 
“Nikiwa hapa shule ya Sekondari Sokoine ningependa kuona na kujiridhisha fedha zilizoletwa na Serikali milioni 700 ambazo zilitakiwa kujenga bwalo la chakula, bweni na jiko kama zimetumika kulingana na mujibu wa BoQ.” amesema Waziri Bashungwa
 
Amefafanua kuwa kulingana na taarifa iliyotolewa,  gharama halisi ya kazi iliyofanyika ni  shilingi milioni 468.15 zikilinganishwa na fedha zilizopokelewa shilingi milioni 700,  hivyo ilitakiwa shilingi milioni 231. 84 ziwe zimebaki.
 
Aidha, wakati akikagua ujenzi wa jengo la huduma ya dharura katika hospitali ya wilaya Mvomero, Waziri Bashungwa ameeleza kutoridhishwa na kuchelewa kuanza ujenzi huo, ambapo Serikali imeshatoa shilingi milioni 300 kutekeleza mradi huo na kuagiza uanze ndani ya kipindi cha siku saba.