Waziri MKuu Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi Watumishi Saba katika halmashauri mbili za wilaya ya Kilombero kwa tuhuma za ubadhilifu wa zaidi ya Shilingi Bilioni 1.3 za makusanyo ya mapato ya ndani.
Mbali na kuwasimamisha kazi Watumishi hao, pia ameagiza watumishi hao warejeshe fedha hizo ndani ya kipindi cha siku Tatu, kabla hajamaliza ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro.
https://www.youtube.com/watch?v=KtNrpML8JWY
Watumishi hao ni pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Ifakara Francis Ndulane anayedaiwa Shilingi Milioni Tano alizoingiziwa katika akaunti yake bila maelezo yoyote.
Waziri Mkuu amewasimamisha kazi Watumishi hao hii leo, wakati wa mkutano wake na Watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Kilombero pamoja na wale wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, akiwa katika siku ya Pili za ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro.
“Mkoa mzima wa Morogoro umekuwa na tatizo la upotevu wa mapato, fedha zinakusanywa zinapita mikononi mwa watu hazifiki benki, hii ni shida, hatutavumilia”, amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Ameongeza kuwa, kwa mujibu wa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika kipindi cha kuanzia mwaka 2016 hadi Juni mwaka huu, Mji wa Ifakara ulikua na makusanyo ya Shilingi Bilioni 2.7 ambapo fedha iliyopelekwa benki ni Shilingi Bilioni 1.9 na kwamba Shilingi Milioni 727 hazijulikani zilipo.
Waziri MKuu amefafanua kuwa, katika mitambo Kumi ya ukusanyaji wa mapato iliyokaguliwa, imeonyesha Shilingi Milioni 348 zilizokusanywa hazikupelekwa benki na hivyo kuishia mikononi mwa watu.
Amesema katika uchunguzi huo ilibainika kuwa fedha hizo ziliingizwa katika akaunti mbalimbali za Watumishi wa halmashauri hizo kutoka kwa Mtendaji wa Kata ya Viwanja Sitini katika Mji wa Ifakara,- Gregory Midas.
Watumishi hao ni Reina Mrema ambaye anadaiwa kuchukua Shilingi Milioni 298, Haile Njitango Milioni 73 na Linus Mdembo anadaiwa kuchukua Shilingi Milioni Mbili.
Wakati wa mkutano huo, Waziri Mkuu Majaliwa ameagiza Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA katika halmashauri ya Mji wa Ifakara, -John Mvanga ambaye ndiye alibaini kuwepo na ubadhilifu wa fedha hizo na baadaye kusimamishwa kazi, arejeshwe kazini mara moja na asibugudhiwe.
“Mlimsimamisha kazi kwa sababu mlijua amegundua madudu yenu, lakini haisaidii, arejeshwe kazini naagiza apewe ulinzi wa kutosha”, amesema Waziri Mkuu.
Kwa upande wa Halmashauri ya wilaya ya Kilombero, Waziri Mkuu amesema kuwa, zaidi ya Shilingi Milioni 600 hazijulikani zilipo huku Shilingi Milioni 98.5 zikidaiwa kuingizwa katika akaunti za Watumishi wa halmshauri hiyo bila maelezo yoyote.
Waziri Mkuu amewataja Watumishi hao kuwa ni Devid Onyango anayedaiwa kuchukua Shilingi Milioni 51, Elakada Kanongole Shilingi Milioni 36, Fork Karunde Shilingi Milioni Nane na Charles Chali anayedaiwa kuchukua Shilingi Milioni 2.5.