Zikiwa zimebaki siku 39 kufika Oktoba 28 ambapo wananchi watapiga kura kuchagua rais, wabunge, wawakilishi (Zanzibar) na madiwani, mchaka mchaka wa kampeni umezidi kupamba moto ambapo leo United People’s Democratic Party (UPDP) imezindua kampeni zake, hafla iliyofanyika Kilwa Kivinje mkoani Lindi.
Akizungumza katika uzinduzi huo, mgombea urais, Twalib Kadege amewasihi wananchi kukichagua chama hicho kwani kimedhamiria kuleta mabadiliko ya kweli nchini endapo kitapata ridhaa ya kuongoza dola.
Akitaja mambo ambayo serikali yake itafanya, Kadege amesema atahakikisha wakulima na wavuvi wananufaika na shughuli zao lakini pia atahakikisha anamaliza migogoro yote kati ya makundi hayo ambayo imedumu kwa muda mrefu.
Aidha, ameweka wazi kuwa serikali yake haitowavumilia wala rushwa, mafisadi na wabadhirifu wa mali za umma watakaopewa adhabu ya kifungo cha miaka 100 jela pamoja na viboko 100, kwani huo ndio utakuwa muarobaini wa kukomesha vitendo hivyo.
Kuhusu maslahi ya watumishi wa umma, Kadege amesema serikali yake itahakikisha kuwa askari wa majeshi mbalimbali wanalipwa shilingi milioni 1.8 pindi tu waingiapo kwenye ajira ili waongeze ari ya kufanya kazi.
Chama hicho pia kimeahidi kulinda muungano na amani ya nchi na kwamba hakitomvumilia yeyote atakayejaribu kuharibu misingi iliyowekwa na waasisi wa mataifa ya Tanganyika na Zanzibar.
Mbali na hayo, chama hicho kimeahidi pia kubadili mfumo wa upatikanaji wa wakuu wa mikoa na wilaya kwa kuwapigia kura, na vyama vyote vitateua wagombea watakaoshiriki kwenye uchaguzi huo.